Mradi wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani, Tanga, Tanzania ni mmojawapo ya miradi mikubwa kutekelezwa nchini Tanzania ambao utagharimu dola za kimerakani 3.5 bilioni sawa na shillingi Trillioni 8 za kitanzania. Mkataba wa mradi huu baina ya nchi ya Uganda na Tanzania ulisainiwa mwezi Mei 2017 na sherehe  za uwekaji jiwe la msingi la mradi zilifanyika tarehe 5 mwezi Agosti 2017, Chongoleani, Tanga. Inatarajiwa kwamba mradi huu utakamilika mwaka 2020.  Bomba hili litakuwa na urefu wa km 1,445 ambapo ujenzi wa km 1,115 za bomba hili utafanyika nchini Tanzania. Bomba hili la kusafirisha mafuta ghafi litapita katika mikoa 8 ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga; wilaya 24 na vijiji 184.

Mradi huu utaleta fursa nyingi za kiuchumi kwa nchi kwa njia ya kodi na mapato mbalimbali lakini pia itatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi pia. Ujenzi wa bomba hili unatarajiwa kuchukua kati ya miezi 24 mpaka 36 na inategemewa kuzalisha fursa za ajira 10,000. Wakati wa kipindi cha uendeshaji wa bomba hili fursa za ajira zinategemewa kufika 1,000. Shughuli za kiuchumi ambazo zinatarajiwa kuwashirikisha watanzania wengi ni pamoja na  biashara za usafirishaji wa bidhaa na watu, ujenzi wa miundombinu mbalimbali, huduma za chakula, uuzaji wa bidhaa za chakula , ulinzi, uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za afya, sheria , fedha, bima, huduma za taka, huduma za ukarabati, vifaa vya usalama kazini n.k.

Baraza linashirikiana na mikoa ambayo bomba hili litapita ili kuhakikisha kwamba mipango madhubuti inaandaliwa ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kushiriki kikamilifu katika mradi huo aidha kwa kupata ajira au kwa kutoa huduma na kuuza bidhaa mbalimbali. Baraza lipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta za umma na binafsi pamoja na wawekezaji ili kuhakikisha uwezo wa watanzania hasa wajasiriamali unajengwa ili waweze kuzalisha bidhaa zenye viwango na kwa wingi ili ziweze kukidhi mahitaji ya wawekezaji. Aidha, Baraza litashirikiana pia na taasisi za elimu kuwajengea uwezo wataalaam mbalimbali hasa wa ufundi ili kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu wa kutosha wa kuweza kufanya kazi katika tasnia ya mafuta na gesi kwa kuwa tasnia hizi zinahitaji ujuzi maalum.

Baraza linatoa rai kwa makampuni ya kitanzania kujiandaa kushiriki katika mradi huu kwanza kwa kuhakikisha kwamba makampuni yao yameundwa na yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na kuangalia uwezekano wa kujiunga pamoja ili kuongeza mitaji na uwezo wa kushiriki katika kutoa huduma au kuuza bidhaaa. Pia mikoa iwaandae watu wao ili waweze kunufaika na fursa zitakazoibuka na mradi huu. Baraza litahakikisha sheria zilizopo zinazohusu ushiriki wa watanzania katka uwekezaji zinatekelezwa na itafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa sheria hizo na mikataba itakayoingiwa na wawekezaji ili kuhakikisha uchumi wa watanzania unakua kutokana na uwekezaji unaofanyika hapa nchini na nchi inanufaika kiuchumi.

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni taasisi ya Serikali iliyoundwa chini ya Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi namba 16 ya mwaka 2004, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Baraza lina jukumu la kusimamia, kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa sera ya taifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004.

Imetolewa na;

Bi. Bengi Issa

Katibu Mtendaji,

10 Agosti, 2017