Habari

Imewekwa: Jun, 04 2018

Waziri Mkuu kutoa tuzo kwa wawezeshaji wananchi Kiuchumi

News Images

Baraza Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linatarajia kufanya kongamano la tatu la wadau wa uwezeshaji wananchi Kiuchumi ambalo litafanyika Juni 18 mwaka huu katika ukumbi wa LAPF mkoani Dodoma lenye kauli mbiu ya ‘Viwanda; nguzo ya uwezeshaji kiuchumi.

Kongamano hilo linatarajia kuhudhuriwa na wadau wa uwezeshaji zaidi ya 400 kutoka kwenye Mawizara, Taasisi za Umma na Sekta binafsi. Lakini pia watakuwepo viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiwemo Mawaziri,Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Ofisi za kibalozi na wasomi wa fani mbalimbali kutoka elimu ya juu na watekelezaji wa shughuli za biashara na uchumi hapa nchini.

Katika Kongamano hilo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mbunge) atakuwa mgeni rasmi na atatoa tuzo za vikombe na vyeti kwa wadau mbalimbali wa uwezeshaji ambao wamefanya vizuri katika kuwezesha wananchi Kiuchumi kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Tuzo hizo za vikombe na vyeti maalum zitatolewa kwa Wakuu wa Mikoa, Wizara, Taasisi za Umma na Sekta binafsi kwa wadau ambao wamefanya vizuri katika utekelezaji wa Sera ya uwezeshaji wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo inaratibiwa na Baraza.

Washindi wa tuzo hizo pia watapewa fursa ya kuzungumzia njia za mafanikio ambazo wamezitumia ili ziweze kuigwa na wadau wengine wa Uwezeshaji kwa mwaka mwingine wa ushindani na kuchochea jitihada za Serikali katika kuondoa tatizo la umasikini kwa kuwaboreshea vipatowananchi ili kumudu changamoto za kimaisha.

Akizungumzia kongamano hilo,Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bibi Beng’i Issa amesema kuwa utaratibu wa kutoa vikombe na vyeti kwa washindi unalenga kuwatia moyo waliofanya vizuri lakini pia kushawishi wadau wengine wa uwezeshaji kufanya vizuri kwa mwaka mwingine wa fedha ili kusaidia Watanzania kuinuka kiuchumi.

“Tunatarajia kufanya kitu cha tofauti katika kongamano hili baada ya kupata uzoefu katika makongamano mawili yaliyopita tutatoa nafasi kwa wajasiriamali waliofanikiwa kueleza wadau wa uwezeshaji njia walizozitumia kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupeana maarifa mapya kuelekea mwaka mwingine wa ushindani’alisema Katibu Mtendaji.

“Ni vema Taifa likawatambua wadau wanaofanya vizuri kwenye uwezeshaji kupitia sekta zote za uchumi kwa lengo la kuwatia moyo na kuchochea kasi ya ukuaji wa Kiuchumi kwani tunahitaji kila Mtanzania aweze kunufaika na fursa za uwezeshaji zilizopo nchini”aliongeza katibu Mtendaji.

“Ni kongamano kubwa litakalotumika kama sehemu ya kujifunza lakini pia kuhimiza Watanzania kuwekeza kwenye sekta ya viwanda ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya amuwa ya tano kuelekea mapinduzi makubwa ya kiuchumi”alisisitiza.

Katibu Mtendaji aliendelea kusema kuwa kongamano hilo pia litatumika kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini sambamba na mifuko ya Uwezeshaji ambayo inatoa dhamana za mikopo na ruzuku kwa vikundi vya uzalishaji mali.

“Tutakuwa na Taasisi za fedha yakiwemo mabenki ambayo kwa namna moja au nyingine yanasaidia kutoa fursa mbalimbali za uwezeshaji kupitia huduma za mikopo kwa wananchi lakini pia wawakilishi kutoka kwenye mifuko ya Uwezeshaji iliyo chini ya Serikali”alisema.

Mheshimiwa Waziri Mkuu siku hiyo pia atazindua taarifa ya uwezeshaji ya mwaka 2017/2018. Taarifa hii imeelezea utekelezaji na mafanikio yaliyopatikana kutoka kwene Wizara, Mikoa na sekta mbalimbali za Umma.

Hii ni mara ya tatu kwa Baraza la Uwezeshaji kuandaa utaratibu wa kutoa tuzo kwa wadau wa uwezeshaji kwani katika kongamano la mwaka jana lililohudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 nafasi ya kwanza kwa upande wa mikoa ilienda Mkoa wa Simiyu huku iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ikiwa kinara upande wa Wizara, Taasisi na Wakala.

Kwenye Sekta Binafsi Benki ya NMB ilikamata nafasi ya kwanza huku mfuko wa TASAF pia ukiongoza kwa upande wa Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Kongamano la mwaka huu litabeba dhana nzima ya jitihada za kuinua uchumi kupitia sekta ya viwanda hivyo kutakuwepo na watoa mada mbalimbali ambao wamebobea kwenye fani hiyo kushirikisha uzoefu wao kwa wadau wa uwezeshaji na washiriki wa kongamano ili kufanikisha maono ya Serikali kuelekea Tanzania ya Viwanda.