Habari

Imewekwa: May, 15 2019

Waziri Mkuu kutambua wadau wa Uwezeshaji

News Images

WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajia kutoa tuzo za vikombe na vyeti kwa Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka kwenye Wizara, Idara, Taasisi za Umma na Sekta binafsi kupitia Kongamano la Nne la Taifa la Uwezeshaji ambalo litafanyika Juni 15 mwaka 2019 katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.

Katika Kongamano hilo ambalo linabeba ujumbe wa ‘Wezesha Watanzania kujenga Viwanda’ Waziri Mkuu pia atazindua ripoti ya Uwezeshaji kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Akizungumza juu ya Kongamano hilo Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Bibi Beng’i Issa amesema kuwa wanatarajia kuwa na kitu cha tofauti kwani mwaka huu idadi ya washiriki ni zaidi ya watu 350 lakini pia kutakuwa na kipengele cha Mjasiriamali bora wa mwaka ambacho hakikuwepo mwaka jana.

“Tumekuwa na utaratibu wa kutoa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri ili kuongeza kasi ya uwezeshaji na kufikia namba kubwa ya Watanzania lakini pia kutambua michango ya wadau ambao wamefanya vizuri kwenye uwezeshaji”alisema Katibu Mtendaji.

Bibi Beng’i aliongeza kwa kusema kuwa wakati wa Kongamano kutafanyika mjadala wa masuala ya uwezeshaji kutoka kwa wabobezi wa masuala ya Kiuchumi ili kusaidia wadau kushirikishana uzoefu kabla ya kuingia kwa mwaka mwingine wa ushindani.

“Tunawakaribisha wadau wote za Uwezeshaji kuhudhuria Kongamano hili ambalo litatoa fursa ya kukuza uchumi wan chi kupitia sekta ya viwanda’alimaliza.

Kongamano la mwaka huu linatarajia kushirikisha Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Taasisi, Mabalozi, vyombo vya habari, wajasiriamali na wadau wa sekta binafsi.