Habari

Imewekwa: May, 15 2019

Watanzania wahimizwa kuchangamkia fursa za bomba la mafuta

News Images

WAMILIKI wa makampuni na watoa huduma mbalimbali wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye mradi wa Bomba la Mafuta ghafi linalotoka Hoima nchini Uganda mpaka Tanga nchini Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Baraza Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’i Issa amewahasa Watoa huduma kujisajili kwenye kanzidata iliyopo Ewura ili wanufaike na zabuni ambazo zitatokana na mradi huo mkubwa hapa nchini.

Bibi Bengi amesema kuwa kasi ya kujisajili imekuwa ndogo kwani mpaka hivi sasa Watanzania waliojisajili kwenye kanzidata hawazidi 350 hivyo amewataka kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hizo.

“Hii ni bahati kwa bomba la mafuta kukatiza hapa nchini hivyo nawaomba Watanzania wajitokeza kwa wingi kujisajili kwenye kanzidata iliyopo Ewura ili waweze kunufaika na zabuni zitakazotolewa’alisema Katibu Mtendaji.

Aprili mwaka jana Baraza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lilifanya Kongamano kubwa katika ukumbi wa Hazina jijini Dar es salaam na kualika makampuni ya ndani ili kueleza fursa zinazopatikana kwenye mradi huo wa bomba la mafuta.

Bomba hilo la mafuta lenye urefu wa 1450 nchini Tanzania litakatiza kwenye Mikoa ya Kagera,Singida, Geita, Shinyanga, Tabora, Tanga, Dodoma na Manyara katika jumla ya wilaya 24 kata 134 litagharimu kiasi cha shilingi Trilioni 8.