Habari

Imewekwa: May, 15 2019

Uwezeshaji vijana nguzo muhimu kuondoa tatizo la ajira

News Images

TAKWIMU ya sensa ya watu na makazi ambayo ilifanyika mwaka 2012 ilionesha kuwa Tanzania kuna idadi ya watu milioni 45 kati yao wanawake ni milioni 23 na wanaume ni milioni 21.9.

Tafiti zilionesha kuwa katika kila watanzania kumi (10) wanne ni vijana ambao umri wao ni kati ya miaka 15 na 35 na asilimia iliyobaki ilienda kwa watoto na wazee ambao kwa kiasi kikubwa ni tabaka tegemezi.

Vijana ndio kada ya wazalishajimali ambao wanahudumia asilimia sitini ya wazee na watoto kwa mujibu wa sensa hiyo.Umri tegemezi bado uko juu sana hapa nchini ukilinganisha na matabaka mengine.

Pamoja na tafiti hizo za kitaalam bado kundi tegemewa la vijana linakabiliwa na matatizo sugu ikiwemo changamoto ya kukosa ajira rasmi na hasa kwa wahitimu waliomaliza mafunzo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali hapa nchini.

Wastani kwa kila mwaka kuna zaidi ya vijana hamsini elfu ambao wanahitimu mafunzo ya elimu ya juu kwa kiwango cha shahada achilia mbali ngazi za stashahada na cheti na wote hawa huingia kwenye soko la ushindani wa ajira rasmi kutegemeana na taaluma zao.Soko la ajira ni dogo kulingana na uhitaji uliopo kwa vijana.

Wachache kati ya wahitimu wa elimu ya juu hujikita kwenye shughuli za uzalishajimali na kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali lakini walio wengi bado wanasumbuliwa na mtizamo hasi wa kutaka kuajiriwa kwenye sekta za Umma na Binafsi.Haya ni makundi mawili tofauti.

Hili kundi ambalo hujikita kwenye uzalishajimali mara nyingi mapenzi ya kujiajiri hutokana na historia nzima ya kaya wanazotoka.Zipo familia ambazo wazazi kiasili ni wajasiriamali hivyo ni rahisi kurithisha tabia hizo kwa vizazi vyao.Watoto wa wafanyabiashara daima huangukia kwenye biashara.

Hivyo basi kuna kila haja kwa hili kundi la vijana wachache ambao hujikita kwenye uzalishajimali likaendelea kuwezeshwa kupitia mifuko na program za Serikali na kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.

Zipo jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na wadau wa Sekta Binafsi ili kunusuru changamoto hii kwa vijana.

Kuna programu za mafunzo zinaendelea kutekelezwa hapa nchini ikiwemo ‘Kijana Jiajiri’ na ‘Kijana Jiandalie ajira’ ambazo zinafanywa na Taasisi ya ushindani ya Ujariamali (TEEC) ambao ni wadau wakubwa wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Lakini pia kwa miaka mitano sasa Baraza la Uwezeshaji limekuwa likiendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana waliomaliza masomo ya elimu ya juu na kuwapa mbegu mtaji ili kuendeleza mawazo yao ya biashara.

Mwishoni mwa mwaka jana Baraza kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi waliendesha mafunzo hayo na kutoa mbegu mtaji kwa vijana watatu ambao walifanikiwa kuibuka vinara kutokana na maandiko bora ya biashara waliyowasilisha.

Katika shindano hilo kijana wa kwanza ambaye anajishughulisha na ufugaji wa mbuzi alipewa mtaji wa shilingi milioni 10 wakati wa pili alipewa hundi ya shilingi milioni 7 huku yule watatu akipewa milioni 5.

Jitihada hizo hazikuishia hapo kwani Baraza pia limekuwa likikabidhi vijana hao kwa wafanyabiashara ambao wamefanikiwa ili kuwaongoza katika miradi ambayo wanaenda kuanzisha.

Mpango huu unaweza kuwa na tija na kupunguza tatizo la ajira lililopo kwa vijana lakini pia unasaidia kuwajengea uwezo waweze kuanzisha miradi yao na kuondokana na dhana ya kutegemea ajira rasmi kutoka sekta za Umma na Binafsi.

Zipo pia fursa mbalimbali za mikopo yenye masharti nafuu na ruzuku kutoka kwenye mifuko ya Serikali ambayo inafika 45 mpaka hivi sasa ambapo kama vijana wakiamua wanaweza kuitumia katika kuanzisha miradi ya pamoja na kuzisogelea fursa hizo.

Serikali ilianzisha mfuko wa vijana katika halmashauri zote sehemu ambazo pia kuna maafisa wa madawati ya uwezeshaji.Vijana pia wanapaswa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye mfuko wa vijana wa Taifa kutoka ofisi ya waziri mkuu.

Akizungumza kuhusu fursa hizo kwa vijana,Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Bibi Beng’i Issa amesema kuwa kuna kila haja kwa vijana kuunda vikundi vya uzalishamali na kuzisogelea fursa zilizopo kwenye mifuko na program za Serikali.

“Huu ni wakati wa vijana kuondokana na mtazamo hasi wa kusaka ajira ni vema wakaunda vikundi vya Kiuchumi na kuisogelea mifuko ya uwezeshaji kwasababu iliyo mingi inalenga watu walio ndani ya vikundi kwasababu wanadhaminika na kufikika kirahisi”alisema Bibi Beng’i Issa.

“Tumekuwa tukiwatia moyo vijana walionufaika na fursa za uwezeshaji kutoka kwenye mifuko ya Serikali kwa kuwatembelea na kuwapa mafunzo na hata ukitazama miradi yao mingi ina uelekeo wa kukua na wengi wao wamendokana na hii ya dhana ya kutaka kuajiriwa”aliongeza katibu mtendaji.

Katika kipindi hiki ambapo Tanzania imedhamiria kuwa na uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda suala la uwezeshaji kwa vijana halikwepeki.