Habari

Imewekwa: Jul, 13 2018

NEEC yawahimiza wahitimu kujikita kwenye ujasiriamali

News Images

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bibi Beng’i Issa amewataka wahitimu wa masomo ya elimu ya juu hapa nchini kuangalia uwezekano wa kujiajiri kupitia biashara na kilimo kwani hivi sasa kuna changamoto ya ajira.

Bibi Beng’i Issa aliyasema hayo wakati wa kufungua semina ya mafunzo iliyoendeshwa na Baraza la Uwezeshaji kwa wahitimu wa ngazi ya shahada katika fani za jinsia na maendeleo kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo jijini Dar es salaam.

“Tunafahamu zipo changamoto kwenye soko la ajira na hasa kwa kada za wasomi kama nyinyi ndio maana tunahimiza utaratibu wa kujiwekea akiba na kuanzisha vikundi vya uzalishajimali kwani mifuko mingi huwafikia watu kwa njia hii”alisema Katibu Mtendaji.

Baraza liliendesha semina ya siku moja ili kuwafunza wahitimu wa vyuo juu ya fursa za mifuko ya Uwezeshaji iliyo chini ya Serikali lakini pia kuwahimiza vijana kuunda vikundi vya uzalishajimali sambamba na kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba.

Mafunzo hayo ya Baraza yaliendeshwa na Mkurugenzi wa Mifuko ya Uwezeshaji Edwin Chrisant na Mkurugenzi wa Uwezeshaji Anna Dominic.