Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeshiriki kikamilifu katika warsha ya siku tatu ya kujengewa uwezo kuhusiana na ushirikishwaji wa wananchi kwa njia ya vikundi ili kuendeleza mradi wa matengenezo ya barabara za vijijini unaoratibiwa na IRRIP (Irrigation and Rural Roads Infrastructure Project).

Maofisa wa Baraza waliambatana na Katibu Mtendaji Bi Beng’i Issa katika warsha hiyo ya siku tatu iliyofanyika mjini Morogoro.

Baraza kama mratibu mkuu wa masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi limeshiriki katika warsha hiyo fupi ili kujadiliana na wadau kuhusiana na namna bora ya kuondoa changamoto za ushirikishwaji wa wanachi katika miradi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo matengenezo ya barabara za vijijini.

Mradi huu unalenga kutengeneza barabara za vijijini na baada ya matengenezo ya barabara hizo wananchi wa vijiji husika wanashirikishwa katika kuzifanyia matengenezo. Mradi huu unatekeleza Ilani ya chama tawala ya kushirikisha jamii ya watanzania walio chini katika manunuzi ya umma. Ambapo asilimia 30% ya manunuzi ya umma itafanywa na akina mama, vijana na watu wenye ulemavu.

Kufuatia utekeleza wa ilani hii Baraza limesaini makubaliano na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), ambapo PPRA tayari imetengeneza mwongozo wa utekelezaji wa suala hili.

Baraza linaamini barabara za vijijini ni moja kati ya maeneo wezeshi ya kuunganisha mawasiliano ya kiuchumi kutoka kijiji kimoja na kwenda kingine hivyo kurahisisha shughuli muhimu za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kuelekea sokoni.

“Tunaunga mkono mradi huu wa ushirikishwaji wa wananchi katika matengenezo ya barabara za vijijini kwani ni moja kati ya maeneo wezeshi yatakayosaidia wanajamii kujipatia kipato na kupunguza wimbi la umasikini, ”alisema Katibu Mtendaji.

“Mradi huu ni vema ukasambaa Nchi nzima kwasababu ndio namna pekee inayoweza kuunganisha barabara za vijijini kuelekea njia kuu za mijini maeneo ambayo masoko ya mazao ya shambani na huduma muhimu za kijamii hupatikana”.

Katika warsha hiyo pia walikuwepo wawakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, bodi ya ukarandarasi nchini (CRB), Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), Tamisemi na Maafisa maendeleo wa wilaya kutoka Halmashauri za Kongwa, Kiteto, Mvomero na Kilombero.

Mradi wa IRRIP unatekelezwa katika wilaya nne ambazo ni Kiteto, Kongwa, Mvomero na Kilombero huku ukiwa na lengo la kusambaa nchi nzima.

Enable Slideshow: 
Enable