Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limetenga kiasi cha shilingi bilioni moja za kitanzania kwa ajili ya kudhamini mikopo inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa Vyama vya Ushirika na Akiba na Mikopo cha Waendesha Bodaboda Nchini.

Mkopo huo unalenga kuwawezesha vyama vya kuweka na kukopa nchini vitakavyoanzishwa na waendesha bodaboda wote  na kwa kuanzia na Chama cha Ushirika na Akiba na Mikopo Waendesha Boda Boda  Dar es Salaam (DABOSA) ili waweze kukua,kuinuka kimtaji na kumiliki bodaboda zao kwa kuwa wengi wameajiriwa kuendesha bodaboda hizo.

Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Beng’i Issa alisema hayo mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano ya kudhamini Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutoa mikopo DABOSA ili iweze kutoa mikopo kwa wanachama wake.

“Fedha hizI za kudhamini mikopo hii zitawekwa kwenye akaunti ya mfuko huo na wao wametenga shilingi tatu kwa ajili ya kazi hiyo” alisema na kuongeza kuwa watatoa mkopo kwa riba ya asilimia 9.32 na DABOSA itatoza kwa wanachama wake kwa asilimia 12.3.

Alifafanua zaidi, Bi. Issa alisema mpango huo ni wa kitaifa wenye lengo la kuwezesha wananchi kiuchumi, hiyo watashirikiana na mfuko huo kuwapatia mafunzo ya utawala bora, kuweka akiba na ujasirimali.

“Mafunzo yameshaanza kutolewa Dar es Salaam na yataendelea kufanyika pia katika mikoa mingine nchini,” alisisitiza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dkt. Ramadhani Dau alisema mikopo hiyo ni njia ya kuwezesha vijana kuondokana na tatizo la ajira ambalo linawakabili.

“Mfuko umejiweka tayari kutoa mikopo hii, lakini jambo la msingi ni kwa vijana waweze kufanya kazi kwa bidii,na kuwa waaminifu katika biashara zao ili waweze kurejesha mikopo,”alisema Dkt. Dau.

Mkurugenzi huyo Mkuu aliwaelezea waendesha bodaboda hao kuwa mfuko unatoa huduma za jamii zikiwemo za mafao ya ajali na mafao ya afya, hivyo wanaweza kujiunga na kunufaika nayo wakati wanaendelea na shughuli zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji,Bw. Omari Issa ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais Utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),alisema programu ya kuwezesha bodaboda ni moja ya mambo ambayo yaliyomo katika BRN.

“Baraza limeondokana na mfumo wa zamani wa kutoa mikopo kwa wananchi moja kwa moja na sasa inadhamini taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wananchi,” alisema.

Alisema wanafanya hivyo na Benki ya Posta, TIB, NSSF na  watashirikiana na taasisi zingine ili kuendelea kuwafikiwa wananchi wengi zaidi.

Mwenyekiti wa DABOSA,Bw. Said Kagomba alisema chama chao ni cha vijana wa jiji la Dar es Salaam kina wanachama 439; Kinondoni (135),Ilala (163) na Temeke (141).

“Lengo ni kuinua,kustawisha na kuboresha hali ya maisha yetu” na mpaka sasa wamekusanya kiasi cha shilling milioni 24.7,”alisema Bw.Kagomba.

Chama kinatarajia kuanza kutoa mikopo kwa wananchama wake kuanzia sasa ambapo utiaji wa saini kati ya Baraza  na NSSF umekamilika.

 

SIFA ZA MAOMBI YA MIKOPO KATIKA MPANGO WA UWEZESHAJI KWA WAENDESHA PIKIPIKI ZA ABIRIA (BODABODA SCHEME) KUPITIA NSSF KWA UDHAMINI WA BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Katika jitihada za kuwawezesha kiuchumi vijana wanaoendesha pikipiki za abiria (Bodaboda), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limesaini mkataba na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Chini ya Mkataba huo NEEC na NSSF watashirikiana katika kuwahamasisha vijana ili waunde vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) ili waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na taasisi hizi mbili. Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na mikopo kutoka NSSF kupitia SACCOS kwa udhamini wa NEEC. Ili kunufaika na mikopo SACCOS zitatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:

A.  SIFA /MASHARTI KWA  SACCOS

 1. SACCOS iwe imesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika
 2. Iwe na Bodi iliyochaguliwa kidemokrasia na kupata mafunzo kuhusu uendeshaji wa SACCOS
 3. Iwe na kamati ya mikopo iliyopata mafunnzo ya namna ya kujadili, kutoa, kusimamia na kufuatilia mikopo yote inayotolewa na chama.
 4. Iwe imejisajili na Baraza na kupata cheti cha usajili wa Baraza.
 5. Iwe na katiba na sera zinazisimamia uendeshaji wa shughuli za chama kama mikopo n.k
 6. Iwe na Kamati ya Usimamizi iliyopata mafunzo ya namna ya kusimamia SACCOS.
 7. Iwe na uzoefu wa kukopeshana usiozidi mwaka mmoja na kuwa na kiwango kizuri cha marejesho kisichozidi asilimia 95.
 8. Iwe na mfumo mzuri wa utunzaji wa kumbukumbu za kiuhasibu za chama.
 9. Iwe na Ofisi inayotambulika.
 10. Utoaji wa mikopo uzingatie taratibu za ushirika kama kuwa na hisa na akiba zinazotosha mkopo unaoombwa na mwananchama.
 11. Muda wa marejesho ya mkopo hautazidi miaka miwili
 12. Iwe tayari kutoa mkopo kwa wanachama kwa riba ya asilimia 12.38 kwa mwaka au asilimia 13.68 kwa miaka miwili
 13. Mikopo kupitia NSSF  itatolewa kwa asilimia 9.38 kwa mwaka au asilimia 10.68 kwa miaka miwili
 14. SACCOS lazima ifungue akaunti benki ya Posta
 15. SACCOS lazima ihakikishe wanachawa wake wamejiunga na NSSF na wanatoa michango yao ya kila mwezi.
 16. Mikopo ya ununuzi wa pikipiki, mwanachama atapewa pikipiki na sio fedha taslimu
 17. Vyombo vya usafiri vitakavyonunuliwa na mkopo wenye dhamana ya Baraza vitakatiwa bima na kampuni yenye mkataba na Baraza.
 18. Mikopo yote itakayodhaminiwa na Baraza itakatiwa pia bima ya maisha ya mkopo.

B.  VIAMBATISHO VYA MAOMBI YA MKOPO

Maombi yote ya mikopo yatapelekwa NSSF na nakala kupelekwa Baraza la uwezeshaji na yatakuwa na viambatisho vifuatavyo;

1. Barua ya maombi ya mkopo (cover letter) ambayo itakuwa imepitishwa na afisa ushirika wa wilaya husika.

2. Muhtasari wa mkutano mkuu wa chama wenye ajenda ya kuomba mkopo NSSF

3. Muhtasari wa Kikao cha Bodi ya chama wenye  ajenda ya kuomba mkopo NSSF

4. Orodha ya waombaji wa mkopo ikionesha;

 • Jina la mwombaji
 • Namba ya uanachama wa SACCOS
 • Namba ya uanachama wa NSSF
 • Kiasi cha hisa kilichopo kwenye akaunti yake
 • Kiasi cha akiba kilichopo kwenye akauti yake
 • Kiasi cha Mkopo unaoombwa
 • Madhumuni ya Mkopo

5. Taarifa ya ukaguzi toka kwa afisa ushirika au Shirika la Ukaguzi la COASCO au mkaguzi anayetambulika na Mrajisi wa vyama vya ushirika.

6.Hati ya Ukomo wa madeni toka kwa Mrajisi Msaidizi wa Mkoa husika

KUDOWNLOAD SIFA ZA MAOMBI YA MIKOPO